MWENYEKITI wa CCM Jakaya Kikwete jana alitumia mkutano wa kampeni kwenye jimbo la Buchosa kujaribu kutuliza wimbi la wanachama wanaohamia vyama vya upinzani kupinga matokeo ya kura za maoni za kupata wagombea ubunge na udiwani, akiwataka waige mfano wake wa uvumilivu.
Alikuwa ameshtushwa na kitendo cha mbunge wa zamani wa Jimbo la Busega, Dk Raphael Chegeni kutoonekana katika msafara ulioenda kumlaki alipowasili na pia kutoonekana kwenye mkutano wa hadhara kwenye jimbo hilo ambalo makada wanne wa CCM wamefungua kesi kumpinga mgombea wa CCM, Dk Charles Tizeba.
Kikwete aliongoza awamu ya kwanza ya kura za maoni za kutafuta mgombea urais wa CCM mwaka 1995, lakini katika amu ya pili aliangushwa na Benjamin Mkapa ambaye baadaye alishinda uchaguzi na kuwa rais wa serikali ya awamu ya tatu.
Kikwete aliingia tena kwenye kinyang'anyiro cha kutafuta urais kwa tiketin ya CCM na kushinda kwa kishindo kwenye kura za maoni za chama hicho mwaka 2005.
Lakini matokeo ya kura za maoni za mwaka huu yamepokelewa kwa hisia tofauti na wagombea na wanachama, huku baadhi wakitangaza kuhamia vyama vya upinzani, wengi wao wakikimbilia Chadema na kwenye jimbo la Buchosa makada wanne wa CCM wamediriki kwenda mahakamani kupinga kitendo cha Tume ya Uchaguzi kumpitisha mwanachama mwenzao.
Mkutano wa kampeni wa rais huyo wa serikali ya awamu ya nne ulikuwa sehemu muafaka ya kuzungumzia mpasuko huo, akiwataka walioshindwa kwenye kura za maoni kutulia kwa kuwa siasa ni ushindani.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Tarafa ya Nyehunge, Kikwete alisema wanachama walioshindwa hawana budi kutulia na kuwapigia kampeni wagombea waliopita kupeperusha bendera ya chama hicho ili kishinde uchaguzi.
Kikwete alimwita jukwaani aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Buchosa, Eric Shigongo akamtaka awasalimie wananchi na baadaye aeleze kuwa atampigia kampeni Dk Tizeba ambaye alishinda kwenye kura hizo za maoni za CCM.
“Huyu ni rafiki yangu; alikuwa anagombea hapa lakini kashindwa. Bwana (alimwambia Shigongo) vumilia kama mimi nilivyovumilia mwaka 1995 wakati niliposhindwa na Mzee Mkapa. Bahati nzuri wewe bado kijana unaweza kusubiri. Sasa uchaguzi umekwisha nataka uwaambie hapa kwamba utamnadi Tizeba,” alisema Kikwete.
Shigongo, ambaye ni mfanyabiashara anayemiliki kampuni ya Global Publishers, aliusamilia umati na kutamka bayana kuwa yuko tayari kumnadi Dk Tizeba katika kampeni za uchaguzi ili ashinde na kuwa mbunge wa Buchosa.
Kikwete alitumia nafasi hiyo kuwasihi wanachama wa CCM kuacha ugomvi akisema siasa ni ushindani na wala si ugomvi na hivyo hawana budi kuunganisha nguvu katika kumsaidia mgombea wa CCM ashinde uchaguzi.
Kikwete alilazimika kuzungumzia mshikamano baada ya kubaini kuwa Dk Chegeni hakuwa miongoni mwa wanachama waliofika kumlaki kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwanza wakati akiwasili juzi, kitu kilichomfanya amwagize mkuu wa mkoa wa Mwanza, Abbas Kandoro, ambaye pia alishindwa kwenye kura za maoni mkoani Iringa, amtafute mbunge huyo wa zamani.
Mbali na Kandoro, agizo hilo pia lilikwenda kwa afisa usalama wa mkoa kuhakikisha Dk Chegeni anapatikana.
Watu hao walifanikiwa kumpata mbunge huyo wa zamani na Kikwete akafanya naye mazungumzo ya faragha juzi jioni kwenye ikulu ndogo ya mkoani hapa
Baada ya kuwasili mkoani Mwanza akitokea jijini Dar es Salaam, Kikwete alikutana na aliyekuwa mbunge wa jimbo la Busega wilayani magu, Dk Raphael Chegeni na kuzungumza naye faragha jioni Ikulu ndogo.
Jimbo la Buchosa pia bado halijakaa vizuri kwa CCM kutokana na makada wanne,
Mgozi Benedict Beligiye, Joa Malima Kasika, Pius Lwamimi na Philmon Sengati kufungua kesi Mahakama Kuu wakidai kuwa iwapo Dk Tibeza ataruhusiwa kugombea ubunge, CCM itakuwa na mgombea mla rushwa.
Katika kesi hiyo namba 40 ya mwaka 2010 iliyofunguliwa kwa hati ya dharura Agosti 18 mwaka huu chini ya Sheria ya Gharama ya Uchaguzi namba 6 ya mwaka 2010, imakada hao wanaitaka mahakama itengue uteuzi huo wa CCM kwa sababu kadhaa, ikiwa ni pamoja na madai kwamba kada mwenzao alijihusisha na rushwa wakati wa kampeni za kura za maoni.
Wakati hali ikiwa hivyo kwenye Jimbo al Buchosa, wanachama wengine sehemu kadhaa wamejitoa CCM na kujiunga na upinzani, akiwemo waziri wa zamani, Arcado Ntagazwa na mbunge wa siku nyingi wa Maswa, John Shibuda ambao wamehamia Chadema.
Wote walishindwa kwenye kura za maoni ambazo ziliripotiwa kutawaliwa na vurugu, rushwa, ukiukwaji wa taratibu huku Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ikikamata wagombea kadhaa, wakiwemo mawaziri na wakuu wa wilaya kwa tuhuma za kugawa rushwa ili kushawishi wanachama.
Akijinadi kwa wapiga kura, Kikwete alisema serikali yake imetimiza ahadi nyingi ilizotoa kwenye uchanguzi uliopita na kusisitiza kuwa yapo ambayo hayajakamilika hivyo iwapo watachaguliwa watayakamlisha.
“Tumejenga barabara ya Usagara hadi Geita kwa kiwango cha lami, tumejenga shule sasa sekondari kwenye kila kata; tuliahidi na tumetekeleza tupeni kura tena wapeni na wagombea ubunge wa Chama cha Mapinduzi pamoja na udiwani” alieleza Kikwete.
Katika hatua nyingine, mratibu wa kampeni za urais za CCM, Abdulahiman Kinana ameeleza kuwa chama hicho hakina mpango wa kubadili ratiba ya mikutano ya kampeni za mgombea wake kwa sababu ya matatizo ya afya ya Kikwete.
Kikwete aliishiwa nguvu ghafla wakati akihutubia kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za CCM uliofanyika viwanja vya Jangwani na ilibidi apewe huduma ya kwanza hapohapo kabla ya kurudi jukwaani kumalizia hotuba yake.
Hali kama hiyo ilimtokea mwaka 2005 wakati akihitimisha kampeni zake kwenye viwanja hivyo na siku hiyo ilibidi akimbizwe hospitalini ambako alipata nafuu na baadaye kuwatoa hofu wanachama kuwa hali yake ni nzuri. Pia aliishiwa nguvu mwaka jana wakati akihutubia kwenye mkutano wa shughuli za kidini kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.
CCM ilieleza kuwa kuanguka kwake kulisababishwa na kuishiwa sukari mwilini, hali iliyotokana na kiongozi huyo kuwa katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani na kwamba hali yake inaendelea vizuri.
Jana, Kinana aliiambia Mwananchi kuwa afya ya Kikwete, ambaye ameshahutubia kwa siku mbili mkoani Mwanza baada ya tukio hilo la Jumamosi, ni nzuri na CCM itaendelea na kampeni zake bila ya kutetereka.
“Afya yake ni nzuri tu naomba (watu) wasiwe na wasiwasi. hatuna mpango wa kumpunguzia muda wala kukatisha ratiba hivyo mikutano yake ya kampeni itaendelea kama ilivyopangwa,” alieleza Kinana.
Leo, Kikwete ataendelea na kampeni zake kwenye mkoa mpya wa Geita ambako atafanya mikutano mitatu na baadaye kuelekea Kagera.
source;- mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

0 comments:
Post a Comment