UGONJWA uliomsababisha David Beckham wa England kukosa fainali za kombe la Dunia Afrika Kusini mwaka huu umevamia Yanga na madaktari wamewapiga 'stop' wachezaji wawili kugusa mpira kwa muda usiojulikana.
Majeruhi hao ni tofauti na mshambuliaji Kenneth Asamoah ambaye ni raia wa Ghana anayesumbuliwa na matatizo ya misuli na leo Jumanne atafanyiwa uchunguzi maalumu na madaktari bingwa wa Hospitali ya Trauma iliyopo Masaki jijini Dar es Salaam ambayo ina mkataba wa kutoa huduma kwa timu hiyo iliyoko makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani.
Wachezaji hao huenda wasionekane uwanjani kwa muda ambao bado haujafahamika ni mshambuliaji Kiggi Makassi na winga Shamte Ally,
Daktari wa Yanga Juma Sufiani ameithibitisha kuwa Shamte anasumbuliwa kwa muda mrefu na msuli mpana wa juu ya kisigino 'Achiles Tendon’ ambao ndiyo ulimzuia Beckham kuchezea England baada ya kuumia katika mechi baina ya timu yake ya zamani ya AC Milan ya Italia na Chievo Verona .
"Hilo tatizo alikuwa nalo tangu msimu uliopita sasa inabidi afanyiwe upasuaji ili kulimaliza tatizo, tunafanya utaratibu wiki hii kufanikisha hilo na nadhani baada ya hapo ndio tutajua atakaa nje ya uwanja kwa muda gani,"alisema Juma ambaye aliwahi kuwa daktari wa Taifa Stars.
"Kiggi yeye vipimo vinaonyesha ana matatizo ya moyo ambayo siyo ya kutisha sana lakini inabidi afanyiwe uchunguzi wa kina wiki hii, ndio apatiwe tiba kamili ambayo nayo hatujajua itatumia muda gani.
"Inabidi nikae na madaktari wa Trauma tuangalie itakuwaje lakini kwa muda huu tumemzuia kucheza mpira kwa muda kwavile inaweza ikamletea madhara lakini akishapewa tiba matatizo hayo yataisha,"alisisitiza Juma na kusema kuwa majeruhi hao wa Yanga hawako katika kiwango cha kutisha bali wanafanyiwa matibabu mapema kuepuka matatizo yanayoweza kujitokeza siku za usoni.
Wachezaji wengine wa Afrika ambao wamewahi kupata matatizo ya moyo ni Fadiga wa Senegal na Kanu wa Nigeria .
0 comments:
Post a Comment