Maalim Seif kushiriki mdahalo

Written By Admin on Wednesday, September 22, 2010 | 11:54 PM

MGOMBEA urais wa Chama cha Wananchi (CUF) visiwani hapa, Maalim Seif Sharif Hamad leo amelazimika kusitisha kampeni zake ili kushiriki mdahalo.

Katika mdahalo huo, wagombea wa urais visiwani hapa, isipokuwa wa Chama Cha Mapinduzi, (CCM) Dk Ali Mohamed Shein, watashiriki.

Kutokushiriki kwa Dk Shein kunatokana na uamuzi wa chama chake kuwakataza wagombea wake na kwamba midahalo yao ni katika mikutano ya hadhara ikiwa ni pamoja na kutangaza mafanikio ya ilani ya 2005/2010 pamoja na ile ya mwaka 2010/2015.

Akizungumza jana visiwani hapa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Demokrasia Kibandamaiti, Kaimu Katibu mkuu wa CUF, Salim Bimani alisema kuwa mdahalo huo utafanyika katika ukumbi wa Bwawani mjini Unguja.

"Kesho (leo) wanaCUF mnatakiwa mtulizane kimya majumbani ili muweze kumsikia na kumuona vizuri Maalim Seif atakapokuwa katika mdahalo utakofanyika Bwawani,'' alisema Bimani.

Bimani alisema kuwa pamoja na mambo mengi Maalim Seif ataulizwa na kujibu maswali papo kwa papo kutoka ukumbini hapo pamoja na kwa njia ya simu kutoka majumbani.

Bimani ambaye pia ni mkurugenzi wa mawasiliano na uenezi, alisema mdahalo huo utaanza saa 4:00 asubuhi.

"Kutokana na mdahalo huo, kampeni za Maalim Seif zitasimama kwa kesho (leo) na zitaendelea kesho kutwa,'' alisema Bimani.

0 comments:

Post a Comment