Lipumba: Nchi iko njia panda

Written By Admin on Monday, August 30, 2010 | 6:39 AM

CHAMA Cha Wananchi (CUF) kimezindua kampeni zake na mgombea wake wa urais, Prof Ibrahim Lip[umba aliwataka Watanzania kuzinduka na kufanya mabadiliko ya uongozi, akisema "nchi iko njia panda".
                 Uzinduzi huo ulifanyika kwenye Uwanja wa Kidongo Chekundu na kuhudhuria na maelfu ya watu ambao hata hivyo hawakufikia idadi ya wafuasi wa chama hicho waliojitokeza kumsindikiza mgombea huyo wa urais wakati akirejesha fomu Tume ya Taifa ya Uchaguzi wiki iliyopita.

Chama hicho, ambacho kinaingia kwenye uchaguzi mkuu kwa mara ya nne tangu kurejeshwa kwa siasa za ushindani nchi, kimesema CCM si chama cha kuendelea kukiweka madarakani kwa kuwa hadi sasa kimeiweka nchi kwenye njia panda.
Prof Lipumba, ambaye pia anawania urais kwa mara ya nne, aliuambia umati huo kuwa nchi inakabiliwa na tatizo la umasikini na kwamba mgombea wa urais wa CCM, Jakaya Kikwete hawezi kupambana na mafisadi ili kuondoa umasikini japokuwa alisema ukizungumza naye ana mipango mizuri.
                 "Trilioni 11 zimekwenda mikononi mwa mafisadi katika kipindi cha utawala wa miaka mitano ya Rais Jakaya Kikwete. Kiasi hicho ni sawa na fedha za bajeti zilizotengwa kwa mwaka huu wa fedha," alisema Profesa Lipumba ambaye aliingia uwanjani hapo akiwa kwenye gari aina ya Toyota Landcruiser lenye rangi ya hudhurungi na ambalo halikuwa na kibati cha namba za usajili.
Profesa Lipumba alisema wakati CCM ikimnadi mgombea wake mwaka 2005, iliahidi kupambana na ufisadi lakini, kilichofanyika ni danganya toto.
Kwa mujibu wa Profesa Lipumba mafisadi wa kweli hawajapelekwa mahakamani na wale wachache waliopelekwa, mashtaka yao yameandaliwa katika njia ambayo serikali itashindwa.
Akizungumzia hali ya maisha ya Mtanzania, Profesa Lipumba, ambaye alionekana kuepuka kutumia mifano migumu ili aeleweke, alisema kila siku Mtanzania yuko kwenye "swaumu ambayo hakunuia".
             "Wananchi wanahitaji kupata milo mitatu kwa siku. Hatuhitaji swaumu zisizo za kunuia kwa kuwa swaumu inahitaji kunuiwa," alisema Profesa Lipumba, ambaye ni mtaalamu wa uchumi.
Akijikita kwenye mifano ya maisha ya kila siku, Profesa Lipumba alieleza kuwa utafiti wa CUF umeonyesha kuwa sukari kilo moja imepanda kutoka Sh500 mwaka 2005 mpaka 1,800 mwaka 2010, wakati unga wa sembe umepanda kutoka Sh250 hadi Sh800 na mchele umepanda kutoka Sh350 hadi Sh1,200.
"Hiyo ni hatari sana," alisema mshauri huyo wa zamani wa kiuchumi wa rais wa Uganda, Yoweri Museveni. 

             Profesa Lipumba alisema ni muhimu wananchi wakaamka kwa kuwa mgombea wa CCM ameshindwa kutekeleza ahadi ambazo alizitoa wakati anagombea urais mwaka 2005.

"Nilimwomba Kikwete tufanye mdahalo kuhusu ilani yao ya mwaka 2005 tuichambue, lakini mpaka leo sijajibiwa. Ninaomba mdahalo huo ili Watanzania waweze kuelewa nini alichokifanya mpaka sasa na sisi tueleze uchambuzi wetu," alisema.
Alisema kwa hali ilivyo, rushwa na ufisadi vinazidi kuongezeka na CUF imekuja na dira ya kupata katiba mpya na kupambana umasikini huo uliokithiri.

"CUF inakuja na dira ya mabadiliko na ndiyo maana nagombea tena," alisema Lipumba.
"Dira yetu ni hii ya kupata katiba mpya yenye misingi ya demokrasia; ufisadi nao umekithiri. Tunahitaji kufanya mabadiliko ili tuunde serikali ya umoja wa kitaifa kupitia katiba itakayotoa haki kwa kila Mtanzania."
Alikejeli kauli mpango wa serikali ya awamu ya nne wa kuboresha kilimo unaokwenda kwa kaulimbiu ya "Kilimo Kwanza", akisema kuwa katika hali halisi ni "kilimo mwisho" kwa kuwa hakijaandaliwa mazingira ambayo alisema ni ya kuboresha kilimo, akiita hatua hiyo kuwa "kilimo bora" na kuboresha sekta ya viwanda.

Profesa Lipumba alitaja tatizo jingine linaloikabili nchi kuwa ni ukosefu wa umeme. Alisema nchi haina umeme wa uhakika kitu ambacho si sawa na hakiwezi kulifanya taifa lijikomboe kutoka kwenyea umaskini.
"Tunahitaji kuboresha miundombinu ya reli ambayo hivi sasa inakufa pia bandari ni ya kuboreshwa ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa," alisema Lipumba.

Prof Lipumba, ambaye alikuwa akishangiliwa wakati wa hotuba yake, alirejea kusisitiza mpango wa chama chake wa kuunda serikali makini ambayo itaweza kutoza kodi ya kukuza uchumi kwa kuwa ilani yao ya uchaguzi inaeleza hivyo.
            Profesa Lipumba alizungumzia mpango wa kutenga nusu ya bajeti kwa ajili ya kuboresha elimu na sekta ya afya, akisema serikali yake itaweka mkakati wa kutumia Sh25 kwa kila Sh100 na katika sekta ya afya atatumia Sh15 kwa kila Sh100.
"Mama mjamzito asiyekuwa na lishe bora ni sawa na kumhukumu mtoto atakayemzaa. Kina mama wajawazito wanahitaji kupata virutubisho; kuna walemavu wengi wanahitaji kusaidiwa na vile vile kuna wazee wastaafu ambao wanalipwa fedha kidogo, kitu ambacho si sawa," alisema.
Alisema CUF imejidhatiti kuhakikisha inaboresha hayo itakapoingia madarakani kwa kuwa mabadiliko yanahitajika na elimu bora inahitajika tangu shule ya msingi.

Lakini aliyesisimua zaidi wanachama na wafuasi hao wa CUF, alikuwa ni mgombea mwenza wa urais, Juma Duni Haji ambaye alitumia maneno makali wakati fulani na yenye kumasha hisia na mifano ya kuchekesha, akifikia hatua ya kufananisha ahadi za mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete na ahadi za Abunuwasi, akisema huzitoa wakati hana uwezo.
Abunuwasi ni muhusika kwenye kitabu cha hadithi cha "Hekaya za Abunuwasi" ambaye anajulikana kwa vituko na mambo yasiyowezekana.
"Amekuwa akitoa ahadi na anaendelea kutoa, lakini mwisho wa siku huwaambia wananchi kuwa tutapata msaada kutoka Marekani sasa hiyo si ahadi hewa?" alihoji Juma Duni, ambaye aliteuliwa na Kikwete kuwa mbunge katika moja ya nafasi kumi ambazo rais amepewa kuteua wabunge.
Duni alisema watakwenda mikoani kuwauliza wananchi ahadi ngapi ambazo mgombea huyo wa CCM ametekeleza tangu alipoingia madarakani mwaka 2005.
Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni hizo, naibu katibu mkuu wa CUF Bara, Joram Bashange alisema chama hicho kitafanya kampeni zake za chini na kumasha hisia za watu aliposema "kwenye jukwaa hataanguka mtu".
"Tutapiga kampeni chini kwa chini na kwenye jukwaa hili haanguki mtu; tuko na Said Miraji kama kampeni meneja wetu," alisema Bashange.

Mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam ulianza majira ya saa 7:00 mchana na kumalizika saa 11:55 jioni.
Mgombea urais wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alifika Uwanja wa Kidongo Chekundu saa 9:49 alasiri akiongozana na mgombea mwenza wa chama hicho, Juma Duni Haji.

Profesa Lipumba alianza kuhutubia majira ya saa 11:23 jioni, muda ambao wafuasi wengi walionekana kuchoka na hivyo kutofuatilia vizuri hotuba yake na baadhi walianza kuondoka wakati muda wa futari ulipokuwa unakaribia.
Mkutano huo uliopambwa kwa vikundi vya kwaya, ngoma na matarumbeta.

0 comments:

Post a Comment