WAKATI Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa akitaka CCM kuacha kutumia mabango ya mgombea urais wa chama hicho yenye picha za Ikulu, chenyewe kimetunisha misuli kikisema hakitaondoa mabango yake kwani hakuna picha za taasisi hiyo nyeti ya nchi.
Mvutano huo umekuja siku moja baada ya Baraza la Vyama vya Siasa, kutaka CCM iache kutumia nyenzo za Ikulu yakiwemo mabango ambayo picha zake zimeandaliwa kwa gharama za Ikulu.
Hata hivyo, akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Makamba alifafanua mambo matatu ya msingi kuhusu mabango ya mgombea urais wa chama hicho Jakaya Kikwete.
Mtendaji huyo mkuu wa CCM, alifafanua kwamba, katika orodha ya mabango yaliyopo hakuna hata moja lenye picha ya Ikulu na kusisitiza, "Kama lipo njoo sasa hivi (jana asubuhi) ofisini, ili twende ukanionyeshe lilipo."
"Hakuna bango lenye picha ya Ikulu, liko wapi? Naomba hili jambo lizungumzwe watu wakiwa wanalielewa vema. Wewe umeliona wapi hilo bango lenye picha ya Ikulu?"
Makamba alipoelezwa kuhusu taarifa hiyo ya Msajili alisema, "Sikiliza bwana, sisi hatukukurupuka tu kuweka haya mabango. Mabango yetu nasisitiza tena yamepata baraka za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec)."
Kwa mujibu wa Makamba, CCM inayo barua kutoka Nec ambayo inaonyesha ruksa ya matumizi ya mabango yote ambayo yalipelekwa tume hiyo kabla ya kuanza kutumika.
"Mimi nazungumza kwa vielelezo bwana, hapa ninayo barua ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo imeruhusu mabango yetu. Hatujakurupuka tu na kutengeneza mabango kisha kuyaweka mitaani," alisisitiza.
Hata hivyo, juzi Mwenyekiti wa Nec Jaji Lewis Makame, alinukuliwa na gazeti dada la The Citizen, akionya kwamba, tume hiyo hiajaruhusu mabango ambayo yanakiuka taratibu.
Lakini, Makamba akizungumzia zaidi suala zima la kusambaa kwa mabango ya CCM katika viunga vya Jiji la Dar es Salaam, alisema chama hicho kina mikataba na kampuni husika ya matangazo.
Aliweka bayana kwamba, mabango hayo yamebandikwa katika maeneo hayo kutokana na makubaliano na kampuni husika ikiwemo Kampuni ya Outdoor, ambayo ni maarufu kwa kazi hiyo.
"Kwa hiyo jambo la tatu na la msingi, haya mabango mnayoona mitaani, CCM imeingia mkataba na kampuni husika kama Outdoor. Msifikiri tumekurupuka tu kuweka haya mabango," aliongeza.
CCM imekuwa na utaratibu wa kuandaa mabango mbalimbali kuhusu mgombea wake wa urais, ambayo humuonyesha akiwa katika matukio tofauti. Karibu mabango yote Dar es Salaam yanamuonyesha Rais Kikwete akiwa katika matukio ya kijamii nje ya Ikulu.
SOURCE;- MWANANCHI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment