Serikali yathibitisha uraia wa Bashe

Written By Admin on Friday, September 10, 2010 | 10:23 AM

WIZARA ya Mambo ya Ndani imemwandikia barua kada wa CCM, Hussein Bashe kuthibitisha kuwa ni raia wa Tanzania baada ya suala hilo kusababisha anyimwe nafasi ya kuwania ubunge wa Nzega kwa tiketi ya CCM.

Bashe alishinda kwenye kura za maoni za CCM kwenye jimbo hilo la Nzega baada ya kupata kura zaidi ya 14,000, lakini akaenguliwa baada ya ukakasi kuibuka kwenye uraia wake.

Baadaye katibu mkuu wa CCM, Yusuf Makamba na katibu wa idara ya itikadi na uenezi ya chama hicho, John Chiligati waliwaambia waandishi kuwa Bashe si raia na kwamba ametakiwa aanze upya taratibu za kupata uraia wa Tanzania.

Alipoulizwa kuhusu suala la Bashe jana, Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha alisema: "Kwa mujibu wa sheria, mimi ndiye wa mwisho kuzungumzia suala hili. Jibu langu lipo pale pale na siwezi kubadili. Bashe ni raia halali wa Tanzania."
Masha, ambaye alishawahi kusema kuwa uraia wa Bashe hauna tatizo, aliongeza kusema: “Nani kasema Bashe si raia? Kama waziri mwenye dhamana nasema, Bashe ni raia halali na hakuna atakayebadilisha msimamo wangu huu.’’

Taarifa ambazo Mwananchi inazo zinasema kuwa barua hiyo ya serikali kwenda kwa Bashe imeandikwa na waziri huyo ambaye pia anasimamia Idara ya Uhamiaji, lakini alipoulizwa na Mwananchi kuhusu barua hiyo hakutaka kueleza chochote zaidi ya kusisitiza kuwa mgombea huyo wa zamani wa ubunge wa Nzega ni raia halali.

Barua ambayo Mwananchi imeiona kutoka kwa mmoja wa maofisa waandamizi wa wizara hiyo inaonyesha kuwa mbali na kumthibitishia Bashe kuwa ni raia, pia imemfafanulia tatizo lililojitokesza kwenye nyaraka za awali kuhusu kabila.

Barua hiyo imeeleza kuwa kwa mujibu wa kifungu Na.5 (1) au 7 (8) cha Sheria Namba 7 ya Uraia ya mwaka 1995, Bashe ni raia wa Tanzania kwa kuzaliwa.

Barua hiyo iliyoandikwa Septemba 3 ambayo inakwenda kwa Bashe, ina kichwa cha habari kisemacho "Upotoshwaji juu ya Uraia wako" ambayo inaonekana kuwa ni majibu ya barua kutoka kwa kada huyo wa CCM akitaka ufafanuzi wa suala lake.

Barua hiyo ya Masha inaeleza kuwa utata kuhusu uraia wa Bashe ulitokana na kada huyo kuwasilisha hati ya kiapo inayoonyesha kuwa ni Mnyamwezi badala ya Mtanzania mwenye asili ya Somalia.

"Utata huo haukuondolei haki yako ya kuwa Mtanzania. Hata hivyo utata huo umeondolewa kwa kiapo kingine ambacho kimerekebisha kile cha awali," anaeleza Masha katika barua hiyo.

"Kwa msingi huo, kwa barua hii ninathibitisha kuwa Hussein Mohamed Bashe Ibrahim ni raia wa Tanzania kwa kuzaliwa kwa mujibu wa Sheria ya Uraia Na.7 ya mwaka 1995 kifungu Na. 5(1) au 7(8)."
Barua hiyo imepelekwa kwa Bashe na kwa katibu mkuu wa CCM, Yusuf Makamba.

Ufafanuzi wa jana wa Masha umetolewa takriban wiki tatu tangu halmashauri kuu ya CCM imuondoe kwenye kinyang'anyiro cha jimbo hilo ambalo lilikuwa linashikiliwa na Lucas Selelii ambaye alishika nafasi ya pili kwa kupata kura zisizidi 3,000 lakini pia akatemwa.

Tiketi ya CCM ya jimbo hilo ilikwenda kwa Dk Khamis Kigwangala ambaye pia alikumbwa na tatizo la uraia baada ya kuhojiwa na Idara ya Uhamiaji na baadaye kuwekewa pingamizi ambalo lilitupwa.

Mbali na kuenguliwa kwenye kugombea ubunge, halmashauri kuu iliagiza mwanasiasa huyo kijana avuliwe uanachama na vyeo vyake vyote ndani ya CCM, ikiwa ni pamoja na ujumbe wa baraza kuu la umoja wa vijana.
Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo la Bashe, katibu mkuu wa CCM, Yusuf Makamba alisema asingeweza kulizungumzia kwa kuwa yuko mapumzikoni.

"Nipo nyumbani kwa mapumziko,'' alisema Makamba na kukata simu.
Naye makamu mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa hakutaka kuzungumzia suala hilo na badala yake alisema: "Mimi nipo Mwanza Vijijini, siyajui ya Dar es Salaam. 

Waulize ambao wako huko (Dar es Salaam).''
Baada ya kikao hicho cha halmashauri kuu ya CCM kilichofanyika Dodoma, Chiligati aliwaambia waandishi wa habari akisema: “Wazazi wa Bashe walikuja nchini wakitokea Somalia na baba yake alipata uraia miaka kumi baadaye. Kwa kuwa Bashe alizaliwa kabla ya wazazi wake kupata uraia, kisheria yeye si raia na kwamba alikuwa akiishi kwa mazoea na matatizo kama haya yamewakumba watu wengi kwa mfano Jenerali Ulimwengu.”

source: mwananchi 

0 comments:

Post a Comment