Siku chahe baada ya mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mabere Marando, kuwahusisha vigogo wa CCM na ukwapuaji wa mabilioni ya fedha za Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), amemshukia Jaji Mkuu, Agustino Ramadhan, akimtaka aache kuikingia kifua CCM.
Marando alisema kama Jaji Mkuu Ramadhan anataka kuingia kwenye siasa, ni vema akanunua sare za chama hicho na kupanda jukwaani kujibu hoja na tuhuma zinazoelekezwa kwa vigogo wa CCM wanaohusishwa na vitendo vya ufisadi.
Baadhi ya vyombo vya habari juzi vilimnukuu Jaji Mkuu akiwaonya wanasiasa akiwemo yeye (Marando) kuwa wanaotoa hotuba za kisiasa majukwaani juu ya kesi zilizo mahakamani wanafanya makosa.
Marando alisema anasikitishwa na kauli hiyo kwa kuwa jaji mkuu si mwanasiasa na hapaswi kusikiliza maneno ya kisiasa na kuyatolea ufafanuzi kama hayajafikishwa mezani kwake.
Alisema katika uzinduzi wa kampeni za CHADEMA, yeye (Marando) alisema watuhumiwa waliofikishwa mahakamani kwenye kesi za wizi wa EPA ni matawi tu na kuwataja baadhi ya vigogo wa CCM ambao walipaswa kuunganishwa katika kesi hizo kwa sababu wao ndio walioubariki wizi huo.
Alisema kauli hiyo si kuingilia mwenendo wa kesi bali kuonyesha kuwa kuna mafisadi wengi ambao walistahili kufikishwa mahakamani, lakini hawajafikishwa kwa sababu ya kinga ya chama au wanatumia madaraka yao.
“Jaji Mkuu anatumia kofia yake kuitetea CCM, anataka jamii ione ninachokifanya mimi na CHADEMA ni kosa, hii si sahihi, namuomba aache kubishana na mimi kuhusu masuala ya kisiasa,” alisisitiza Marando.
Marando alibainisha kuwa kuna chombo kinachoshughulikia nidhamu ya mawakili hivyo kama yeye atakuwa amefanya makosa chombo hicho kitamuita kumuonya na ikiwezekana kumuadhibu lakini si anavyofanya Jaji Mkuu.
“Yeye kama ana hamu ya kupanda jukwaani si akanunue sare ofisi za CCM pale Lumumba ili tuweze kupambana naye kwenye uwanja unaostahili?” alisema Marando.
Aliongeza kuwa Jaji Mkuu ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, hivyo ana uwanja mpana wa kutolea uamuzi au ufafanuzi kesi inayopelekwa mezani kwake na si maneno yanayosemwa katika viwanja vya Jangwani au vinginevyo katika kampeni zinazoendelea hivi sasa.
Alisema ufisadi ni hoja nzito ambayo haipaswi kupindishwa pindishwa au kutetewa na viongozi kwa sababu imewafanya Watanzania waendelee kuwa maskini katika ardhi yao, huku watu wachache wakitumia rasilimali za nchi kwa maslahi binafsi.
Aliongeza kuwa kutokana na kutambua athari za ufisadi, CHADEMA imeamua kuuvalia njuga na kuwaumbua wale wote walioshiriki au wanaoendelea kutenda vitendo hivyo.
Marando amshukia Jaji Ramadhani
Written By Admin on Friday, September 3, 2010 | 8:28 PM
Labels:
POLITICS,
UCHAGUZI 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment