Taifa Stars kila la kheri

Written By Admin on Friday, September 3, 2010 | 3:42 PM

TIMU ya Taifa 'Taifa Stars', leo itatupa karata yake ya kuwania kucheza fainali za Mataifa ya Afrika ugenini dhidi ya Algeria.



Mechi hiyo itakuwa nafasi nzuri kwa kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mdenmark Jan Poulsen kusaka tiketi ya kushiriki michuano hiyo ambayo kwa mara ya mwisho, Tanzania ilishiriki miaka ya 80 nchini Nigeria.


Kutokana na umuhimu wa michuano hiyo, Stars inatakiwa kuifunga Algeria nyumbani kwao ili ijiweka katika mazingira mazuri ya kundi lao lenye timu nyingine za Morocco na Jamhuri ya Afrika ya Kati.


Pamoja na maandalizi yaliyoafanywa kwa timu hiyo chini ya kocha Poulsen, kinachotakiwa ni kuzingatia yote waliyoifundisha na kuyafanyia kazi uwanjani.


Pia, Watanzania tunatakiwa kuelekeza maombi yetu nchini Algeria ambako kikosi cha Taifa kitakuwa kikipeperusha bendera ya Taifa ili kirejee nyumbani kikiwa na ushindi.


Mchezo wa kwanza ni muhimu kwa timu yoyote, kwani huwaondoa hofu wachezaji katika mechi itakayofuata na hata mashabiki kuwa na imani na timu yao katika mechi zitakazofuata.


Kikubwa kinachotakiwa kwa vijana wetu, ni kuwa na nidhamu uwanjani, kujituma na kuhakikisha hawawapi nafasi ya kumfikia kipa wapinzani wao.
Pia, wakumbuke kwamba, kikosi hicho kiliweza kuzitikisa Burkina Faso, Ivory Coast, Senegal na Cameroon, hivyo Algeria isiwatishe kwa kuwa ilishiriki fainali za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini.

Imani yangu ni kwamba, kama wachezaji wa Stars wakiacha hofu ya kucheza na timu hiyo, wana uwezo wa kuifunga nyumbani kwao ama kuibana na kutoka nayo sare.


Mashabiki wa soka, tuungane katika kuiombea dua Stars ili iweze kushinda mechi hiyo muhimu ugenini kabla ya kurejea nyumbani na kuwasubiri.

0 comments:

Post a Comment