
Akihutubia maelfu ya wananchi katika “viwanja vitakatifu vya Jangwani,” kabla hajaishiwa nguvu na kudondoka chini, jijini Dar es Salaam, Jumamosi iliyopita, Kikwete alidai serikali yake imefanya mengi.
Viwanja hivi vinaitwa vitakatifu kutokana na kuwa sehemu ambako Papa Yohana alifanyia ibada pale alipotembelea Tanzania. Aidha, hapo ni mahali ambako madhehebu ya Kikristo yamegeuza kuwa mahali pa kufanyia mahubiri,
Rais Kikwete aliuambia umati kwenye viwanja hivi wakati wa kuzindua kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa serikali yake imepambana kikamilifu na rushwa. Akasisitiza, “katika hili hakuna anayeweza kutunyoshea kidole.”
Akatoa mfano wa kesi kadhaa zilizofunguliwa mahakamani, kama kielelezo cha utekelezaji wa kile alichokieleza.
Lakini wote tunajua kuwa wengi waliofikishwa mahakamani ni “dagaa wa rushwa” huku mapapa wa rushwa wakiendelea kutamba. Baadhi yao, wamepitishwa na chama chake kugombea ubunge.
Tunajua pia kwamba baadhi ya hao waliofikishwa mahakamani, ni wale waliokataa kumuunga mkono mwaka 2005 alipokuwa anausaka urais.
Wengi waliofikishwa mahakamani, walikuwa nje ya kundi la “mtandao” uliomuingiza madarakani.
Ndiyo maana baadhi ya wanaojua kinachoendelea wanasema mtu kama Jeetu Patel, ambaye alifikishwa mahakamani kwa tuhuma za wizi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), alikuwa mfuasi wa mzee John Malecela, aliyekuwa tishio kuu la Kikwete.
Haohao ndio wanashangaa kuona wafanyabiashara wa aina ya Rostam Aziz, anayehusishwa na tuhuma za wizi wa mabilioni ya shilingi kupitia kampuni ya Kagoda, hadi sasa hajafikishwa mahakamani, na hakuna dalili ya serikali kufanya hivyo.
Na imesemwa mara kadhaa na watu wanaojua vema siri ya wizi huo, kwamba mabilioni hayo yaliyokwapuliwa, pamoja na mambo mengine, yametumika kumuingiza Kikwete madarakani.
Serikali ya Kikwete huyohuyo ndiyo imenukuliwa ikisema, mara kadhaa, kwamba “Kagoda hakamatiki.”
Si hivyo tu. Kikwete ndiye anaongoza chama ambacho kimeshindwa kuwachukulia hatua watu kama Andrew Chenge, aliyewahi kuwa mwanasheria mkuu wa serikali.
Chenge ametajwa katika mambo kadhaa, ikiwamo ununuzi wa rada ya kijeshi, mikataba ya madini, ukodishwaji wa shirika la Reli la Taifa (TRC), uuzaji wa Shirika la Ndege la Taifa (ATC), benki ya NBC, mashamba na migodi.
Lakini katika mazingira ambayo ni Kikwete pekee mwenye kujua undani wake, Chenge huyuhuyu ndiye kinara wa kamati ya maadili ya CCM.
Pamoja na majigambo kuwa serikali ina mkono mrefu, lakini Kikwete ameshindwa kufikisha mahakamani gavana wa BoT, Dk. Daudi Ballali, anayekabiliwa na tuhuma za wizi wa fedha za umma.
Badala yake, serikali imefikisha mahakamani wafanyakazi wa ngazi ya chini wa BoT, kwa kile kinachodaiwa, “kushirikiana na baadhi ya watuhumiwa.”
Amemshindwa Dk. Idris Rashid, mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), ambaye anatajwa katika kashifa ya rada, wizi katika EPA na ushawishi wa ununuzi wa mitambo chakavu ya kuzalisha umeme kutoka kampuni ya Richmond?
Ni Kikwete huyuhuyu aliyejipa mamlaka ya kuhukumu na kusamehe wezi wa EPA, aliposema “watakaorejesha fedha watasamehewa.”
Ingawa hatujui kama fedha zilirejeshwa kweli, hakuwachukulia hatua waliosemekana kurejesha fedha hizo. Huku ndiko kupambana na rushwa?
Kama Kikwete alikuwa na dhamira safi ya kupambana na rushwa, mbona ameshindwa kufuta wanachama wenzake walioshinda uchaguzi kwa kutumia rushwa?
Mbona ameshindwa kusikiliza rufaa za wagombea waliolalamikia vitendo hivyo? Mbona amepuuza malalamiko ya wanachama na wazee wa chama chake waliokuwa wanamtuhumu katibu mkuu wake, Yusuph Makamba kwamba anavuruga uchaguzi?
Katika mazingira haya, rais anapata wapi ubavu wa kusema amepambana na rushwa? Anapata wapi ujasiri na majigambo? Anataka kumdanganya nani, kwa faida ipi? Nani atamuamini?
Wala hakuna mashaka, kwamba chini ya utawala wake, kila kitu ndani ya CCM kimehalalishwa. Mwenye fedha ameruhusiwa kucheza rafu; akiishapita katika kura za maoni, kazi imekwisha.
Ni udhaifu huu wa Kikwete uliokifanya chama chake kuwa gulio la uhalifu. Ushahidi wa hili, ni hatua yake ya kukumbatia hata wale waliohusika katika wachafua viongozi wenzake katika chama na serikali.
Mfano hai, ni hatua ya Kikwete kukumbatia baadhi ya waandishi wa habari walioshiriki kumchafua Dk. Salim Ahmed Salim mwaka 2005.
Hadi sasa, Dk. Salim bado anatafunwa na dhambi hii ya mtandao wa Kikwete; itachukua muda mrefu kusahau, hata kama anaweza kusamehe.
Katika mkutano wa Jangwani, mbali na kujigamba kupambana na rushwa, Kikwete alijadili pia suala zima la usalama wa raia na mali zao.
Wakati Kikwete anasema, serikali yake imeimarisha ulinzi na usalama wa raia, Watanzania bado wanakumbuka jinsi majambazi yanavyoteketeza maisha ya wananchi.
Ni majuzi tu, Profesa Jwan Mwaikusa alipigwa risasi na kuuawa katika mazingira tatanishi. Ndugu na marafiki wa marehemu waliopatwa na misukosuko hiyo wanamwelewaje Kikwete?
Bila aibu, Kikwete anasema serikali yake imesimamia uhuru wa vyombo vya habari. Je, imesimamiaje uhuru huo bila kufuta sheria kandamizi? Mbona imekataa katakata kutunga sheria ya uhuru wa habari, licha ya wadau kuisaidia kuipitia na kutoa mapendekezo kwa miaka minne sasa?
Mbona baadhi yetu tumeendelea kusakamwa na kushambuliwa? Mbona Idara ya Habari (MAELEZO) imeendelea kutisha waandishi na vyombo vya habari vinavyoikosoa serikali yake?
Mbona serikali yake imeendelea kununua waandishi? Mbona hata juzi alipoanguka jukwaani, watu wake walikuwa wanahaha kuzuia televisheni zisirushe habari ya kuanguka kwake?
Mbona watu wake walikamata waandishi wa habari, eti kwa kuwa walikuwa wanapiga simu kutoa taarifa ya tukio hilo? Hapa napo, anamdanganya nani?
Vitisho dhidi ya vyombo vya habari na waandishi wa habari mmojammoja, vimeimarika siku hadi siku. Kila uchao, Watanzania wanashuhudia serikali inavyotumia ubabe wa kunyima baadhi ya vyombo matangazo kwa shabaha ya kuvilainisha, kulainisha waandishi wa habari na wamiliki wake.
Hata msafara wake wa kampeni, umetawaliwa na mtazamo huo. Baadhi ya magazeti ambayo yamekuwa yakiikosoa serikali, yametengwa katika kampeni zake.
Kielelezo kikuu cha serikali kukosa dhamira njema na vyombo vya habari, ni kule kufungia baadhi ya magazeti na kuendelelea kung’ang’ania sheria kandamizi ya magazeti ya mwaka 1976.
Jingine ambalo Kikwete alijitapa kuwa serikali yake imeimarisha, ni Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Alisema “mambo mengi yaliyokuwa yana utata yamepatiwa ufumbuzi na kwamba yaliyobaki ni machache na yanaendelea kushughulikiwa, Watanzania bado ni wamoja."
Lakini hajasema, hicho anachoita ufumbuzi ni kipi? Nani asiyejua kuwa muungano huu umeendeleaa kuzorota?
Kwa mfano, mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ambayo yameweka msingi mkuu wa kisheria wa kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa, yamechomekwa mambo mengi, ikiwamo kuirudishia Zanzibar hadhi yake kama nchi.
Kikubwa kinachotatiza katika muswada huo ni hiki: Marekebisho hayo yamerejea kulekule tulikotoka. Yameitambua Zanzibar kuwa nchi, ikiwa na mipaka yake kama ilivyokuwa kabla ya Muungano mwaka 1964.
Huu ndio msingi wa wale wanaomkosoa Kikwete: Je, Zanzibar itakuwaje huru, ndani ya Muungano wa nchi mbili zilizoamua kuachia mamlaka ya kuwa nchi moja – Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?
Hata hivyo, hilo lililofikiwa Zanzibar halikutokana na matakwa ya Kikwete, bali uasi wa Rais Amani Abeid Karume, baada ya kubaini janjajanja ya Kikwete na Makamba katika kamati ya mwafaka.
Mpaka hapa Kikwete anaweza kusema kuwa amefanikiwa kupunguza matatizo katika Muungano?
Kingine kinachothibitisha kuwa muungano unayumba, ni usiri wa jinsi muswaada ulivyopitishwa. Iliilazimu serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kusubiri hadi Bunge la Jamhuri limalize mkutano wake, ndipo mswaada ufikishwe barazani.
Karume na serikali yake walisubiri CCM imalize mikutano yake ya Kamati Kuu (CC), Halmashauri Kuu (NEC) na mkutano mkuu, ndipo mswaada wa kuifanya Zanzibar kuwa taifa huru ulipowasilishwa.
Kama Kikwete na serikali yake wangeweza kumaliza matatizo ya Muungano, kuviziana huku kungetoka wapi?
Aidha, mabadilko hayo yameongeza mamlaka ya kiutendaji kwa rais wa Zanzibar katika kuunda mikoa na wilaya.
Kimsingi, marekebisho hayo yanagongana moja kwa moja na Ibara ya 2 (1) na (2) ya Katiba ya Jamhuri inayofafanua eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katiba hii ndiyo iliyoweka madaraka yote ya ugawaji maeneo kwa rais wa Jamhuri. Mabadiliko yamepora madaraka ya rais wa Jamhuri na sasa madaraka hayo yamekabidhiwa kwa rais wa Zanzibar kinyume na katiba.
Katika hili, Kikwete asipoangalia vema, atakuta anakuza matatizo ya Muungano badala ya kuyatatua. Kwani inaeleweka kuwa si rahisi kubadili katiba ya Zanzibar bila kuathiri katiba ya Muungano.
Katiba ya Muungano haitambui makamu wa rais wawili wa Zanzibar . Ile ya Zanzibar imewaingiza na kuwatambua. Je, Kikwete haoni utata huo? Anaendelea tu kujigamba.
Hadi hapa, tambo za Kikwete hazina mashiko.
SOURCE; MWANA HALISI na Saed Kubenea
0 comments:
Post a Comment