WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha ambaye alitangazwa kupita bila kupingwa, sasa amepata mpinzani katika harakati zake za kuwania ubunge jimbo la Nyamagana, mkoani Mwanza.Habari zilizolifikia jana zimeeleza kuwa Masha amepata mpinzani baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kutengua pingamizi lake lililomwondoa kwenye kinyang'anyiro hicho mgombea wa Chadema, Ezekiel Wenje.
Kutokana na uamuzi huo wa Nec, Chadema jana ilifanya sherehe kubwa jimboni humo kufurahia matokeo hayo yanayoweza kubadili mwelekeo wa siasa za ubunge jimboni humo.
Mwenyekiti wa kamati ya wagombea wa Chadema, Dadi Igogo aliliambia gazeti hili jana kuwa wamepokea uamuzi huo wa kwa furaha na kwamba, sasa wanajipanga kupata ushindi.
"Tunafurahi kwa uamuzi huo kwa kuwa sasa imebainika kuwa ushahidi uliotolewa na mlalamikaji kuwa Wenje sio raia haukujitosheleza," alisema Igogo.
Alisema Chadema ilikuwa na wagombea 182,sita waliondolewa kwa pingamizi na wamebaki 176.
"Hukumu iliyolewa leo inaweza kuwa mwanzo mpya wa kuwarejesha wagombea wetu wote walioondolewa kwa pingamizi," alisema Igogo.
Masha anayewabua jimbo hilo kwa kipindi cha pili, alimwekea pingamizi Wenje kwa maelezo kuwa sio raia wa Tanzania.
Pingamizi hilo lilikubaliwa na Msimamizi wa Uchaguzi jimboni la Nyamangana na Wenje alikata rufaa Nec kupinga uamuzi huo uliyomfanya Masha kuwa mgombea pekee.
Msimamizi wa Uchaguzi wa jiji la Mwanza, Willson Kabwe, alitangaza Wenje ameenguliwa kuwa mgombea katika jimbo hilo kutokana na kukosa sifa ya uraia na kudanganya makazi.
Lakini jana Wenje aliliambia gazeti hili kuwa Nec ilitupa maamuzi ya msimamizi huyo na kumrejesha tena kwenye kinyang'anyiro hicho.
"Nimefahamishwa na Mwanasheria Mwandamizi wa Serikali iliyejifahamisha kwa jina la Kavishe kwamba nikachukue barua ya uteuzi wa kuwa mgombea,"alisema Wenje.
Wenje ambaye aliahidi kukutana na waandishi wa habari leo kuzungumzia uteuzi huo alisema anafurahi kuona Nec imegundua kuwa haki haikutendeka katika uamuzi wa awali.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika jana aliliambia gazeti hili kuwa ni kuwa kweli Wenje amerejeshwa kwenye kinyang'anyiro cha ubunge jimbo la Nyamagana.
"Nimesikia lakini, Nec ndio wanapaswa kutoa taarifa, au mgombea mwenyewe anaweza kufanya hivyo," alisema Mnyika.
Mkurugenzi wa Nec, Rajab Kiravu alisema kuwa tume hiyo ya uchaguzi, haiwezi kutoa taarifa ila mgombea mwenyewe akiona inafaa.
"Tume haiwezi kuzungumzia hilo, atafutwe mgombea mwenyewe,"alisema Kiravu.
Akizungumzia uamuzi huo Masha alisema kuwa anamkaribisha Wenje ulingoni ili waende kupambana, kwani anaamini kuwa atashinda.
"Namkaribisha sana ulingoni na tupambane nitamshinda na hakuna kingine,"alisema Masha.
Alisema kuwa uamuzi wa tume ni uamuzi, atauheshimu na hana cha kusema zaidi ya kusubiri mapambano.
SOURCE; MWANANCHI
Waziri Masha apata mpinzani
Written By Admin on Thursday, September 2, 2010 | 4:47 PM
Labels:
POLITICS,
UCHAGUZI 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment