HOTUBA YA MH. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE BARAZA LA EID-EL-FITR, DODOMA,
Mheshimiwa Sheikh Issa bin Shaaban Simba, Sheikh Mkuu
na Mufti wa Tanzania,
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa,
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya BAKWATA;
Wajumbe wa Baraza la Ulamaa;
Waheshimiwa Masheikh na Viongozi wa BAKWATA;
Waheshimiwa Viongozi wa Dini wa
Madhehebu Mbalimbali;
Viongozi Wenzangu wa Chama na Serikali;
Ndugu Wananchi; Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana;
Assalaam Ellaykum Warahmattullah Taallah Wabarakatuh!
Eid-Mubarak!!
Nakushukuru
sana Mheshimiwa Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania kwa kunialika kuja
kujumuika nanyi katika siku hii adhimu ya kusherehekea kumalizika kwa
mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Naungana na nawe na Katibu Mkuu wa
BAKWATA Sheikh Suleiman Saidi Lolila kumshukuru Allah Subhana Wataalah
kwa kutuwezesha kufunga na kutimiza moja ya nguzo tano za Uislamu.
Inshaalah tuzidi kumuomba Mola wetu aendelee kutujaalia uhai na uzima
ili tuweze kufunga Ramadhani ijayo na za miaka mingi ijayo.
Mheshimiwa Mufti wa Tanzania;
Naungana
nawe pia, kuwapongeza Waislamu wote nchini na duniani kwa kumaliza
salama ibada ya swaumu kwa mwaka huu. Inshaalah tuombe kwa Mwenyezi
Mungu sote tuwe miongoni mwa wale ambao funga zao zitakuwa zimekubaliwa.
Aidha, tuombe tuwe miongoni mwa waja wake ambao toba zao zimetakabiliwa
na kusamehewa madhambi yao na adhabu ya moto.
Napenda nami
nijumuike nawe pamoja na , Katibu Mkuu wa BAKWATA na Masheikh wote
nchini kuwaomba na kuwasihi Waislamu wote nchini kwamba, ucha Mungu
tuliouonyesha katika kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhan usiwe umeisha
jana bada ya kuandama kwa mwezi. Badala yake, hauna budi uwe endelevu,
kwa maana ya sisi kuendelea kutenda mema na kuepuka kutenda dhambi na
mambo yanayomchukiza Mwenyezi Mungu. Katu ucha Mungu siyo kwenye kipindi
cha Mwezi mtukufu peke yake.
Risala
Mheshimiwa Mufti;
Nawashukuru
sana kwa risala yenu iliyowasilishwa vizuri na Katibu Mkuu wa BAKWATA.
Yote mliyosema kuhusu Serikali, nchi yetu, Waislamu na Watanzania kwa
jumla nimeyasikia na kuyaelewa. Napenda kuanza kwa kusema kuwa Serikali
inaunga mkono na inapenda sana kuwa na uhusiano na ushirikiano wa karibu
na mashirika, viongozi na waumini wa dini zote nchini bila ya kubagua
wala kupendelea.
Bila ya shaka mtakubaliana nami kuwa maneno
haya niyasemayo leo si mageni kwako na masikioni mwa Watanzania.
Nimeshayasema mara kadhaa siku za nyuma. Tena haya ni maneno ya dhati na
wala siyo ya kuwapaka mafuta kwa mgongo wa chupa kama msemo wa
Kiswahili usemavyo.
Mheshimiwa Mufti;
Serikali ina
msimamo huo kwa sababu tunatambua na kuthamini sana nafasi na mchango wa
dini na mashirika ya dini katika maendeleo na ustawi wa jamii na nchi
yetu kwa ujumla. Serikali inaunga mkono mashirika ya dini katika
shughuli zao kwa sababu ya manufaa ya dhahiri ya shughuli hizo kwa taifa
letu. Mashirika ya dini yamekuwa mstari wa mbele kushirikiana na
Serikali kuwapatia wananchi wa Tanzania huduma muhimu za elimu, afya,
maji n.k. Bila ya ushirikiano, upatikanaji wa huduma hizo kwa baadhi ya
maeneo ungekuwa tofauti sana. Serikali kwa upande wake imekuwa inafanya
kazi ya kusaidia mashirika ya dini yaweze kutoa huduma hizo kwa
wananchi.
Napenda kuwahakikishia kuwa hakuna kitu cho chote
ambacho Serikali itatoa kwa dini moja ambacho dini nyingine itanyimwa.
Kwa kweli mbele ya Serikali dini zote zina haki sawa. Kama hujaomba
usimlaumu aliyeomba akapewa au aliyempa. Kama yupo anayeamini anazo sifa
kama mwenzake aliyepewa aombe naamini atapewa. Iwapo itafanyika
vinginevyo dai haki yako kwa mamlaka zinazohusika.
Mheshimiwa Mufti, Ndugu Zangu Waislamu;
Maelezo
yangu haya yanafanana na hoja zenu katika Risala yenu kuhusu Itifaki ya
Maridhiano ya 1992 baina ya Serikali na TEC na CCT. Nafurahi kwamba na
nyie mmeamua kuleta maombi, yaleteni yatashughulikiwa ipasavyo.
Mheshimiwa Mufti; Ndugu Zangu Waislamu; Watanzania Wenzangu Wote;
Sababu
ya pili inayoifanya Serikali kuunga mkono madhehabu ya dini katika
shughuli zao ni kazi kubwa yaifanyayo ya kuwalea Watanzania kuwa wacha
Mungu. Sisi tunaamini kuwa kama madhehebu yatafanikiwa kwa hili nchi
yetu itakuwa mahali pazuri sana pa kuishi. Wacha Mungu ni watu wema,
hawatendi maovu, waaminifu, waadilifu, hawaombi, hawatoi wala kupokea
rushwa. Wacha-Mungu ni watu wenye upendo kwa watu wote na daima hupenda
amani, usalama na utulivu. Kwa sababu hiyo mambo mengi maovu katika
jamii na Serikali yatapungua, watu watahudumiwa ipasavyo na hivyo
kuvipunguzia vyombo vya dola kazi ya kupambana na uovu na uhalifu.
Uhuru wa Kuabudu
Sababu
ya tatu, Mheshimiwa Mufti, ni kuwa uhuru wa kuabudu unatambuliwa kuwa
moja ya haki za msingi za raia wa Tanzania katika Katiba ya nchi na
unalindwa kisheria. Watanzania wako huru kufuata na kuabudu dini yoyote
waipendayo au kutokukufuata dini yoyote. Tanzania haina dini ya taifa au
ya Serikali ambayo watu wote lazima waifuate. Aidha, hairuhusiwi
kisheria kubeza au kudharau dini au imani ya mtu mwingine na hata nyumba
za ibada. Imefanywa hivyo makusudi kwa nia ya kulinda uhuru wa watu
kuabudu na kudumisha amani katika jamii na nchini. Naamini kama ingekuwa
kinyume chake amani ingeweza kuvunjika.
Mheshimiwa Mufti, Waheshimiwa Masheikh na Watanzania Wenzangu;
Inasikitisha
kusikia kuwa wapo viongozi na waumini wa dini zetu nchini wakipita huku
na huko na wakati mwingine wakitumia nyumba za ibada kuhubiri kejeli
dhidi ya dini nyingine. Kukashifiana hujenga chuki na uhasama baina ya
waumini wa dini mbalimbali na kuhatarisha amani na usalama. Hivi
viongozi wangu wa dini, hamuwezi kueneza imani ya dini zenu bila
kukashifu dini ya wenzenu. Kama kweli wewe ni kiongozi wa dini
unaetambua wajibu wako ipasavyo, huwezi kufanya hivyo na wala huhitaji
kukumbushwa na Polisi kutokufanya hivyo. Tafadhali acheni na mamlaka
husika acheni ulegevu kusimamia sheria. Ajizi yenu inaweza kuleta maafa
katika taifa. Timizeni wajibu wenu ipasavyo bila woga wala kuonea au
kupendelea.
Pamoja na hayo ni vyema viongozi wa dini zote na
madhehebu yote mkafufua na kuendeleza utaratibu mzuri uliokuwepo siku za
nyuma wa mawasiliano baina ya dini mbalimbali. Itasaidia sana
kuzungumzia masuala ya namna hii na hata la uadui mlilolitaja katika
Risala yenu. Nguvu ya dola peke yake si jawabu.
Hoja za Risala
Mheshimiwa Mufti; Ndugu Zangu Waislamu,
Katika
risala yenu mmezungumza mambo kadhaa mengine na kutoa ushauri mzuri
ambao napenda kuwahakikisha kuwa tutaufanyia kazi. Hata hivyo,
niruhusuni niyazungumzie au kutoa ufafanuzi kwa baadhi ya mambo.
Mahujaji
Mheshimiwa Mufti,
Napenda
kukupongeza wewe na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kwa kazi
kubwa na nzuri muifanyayo kuhusu upelekaji wa mahujaji Makka na Madina
kila mwaka. Ni kweli kabisa kwamba BAKWATA inayo rekodi nzuri ya
kuwasafirisha, kuwahudumia na kuwarejesha salama nyumbani mahujaji.
Napenda kuwatia moyo kuwa muendelee kufanya vizuri zaidi mwaka hadi
mwaka ili BAKWATA iwe chaguo la hiari la Waislamu wanaotaka kwenda
kutimiza ibada ya Hija.
Pamoja na hayo, zipo taarifa za baadhi
ya taasisi zinazoshughulikia upelekaji wa mahujaji kutokufanya vizuri.
Matokeo yake mahujaji wamekuwa hawahudumiwi ipasavyo na safari ya Hija
hugeuka kuwa adha badala ya kuwa furaha shangwe. Je, hamuoni umuhimu wa
jambo hili kulitengenezea vigezo fulani ambavyo kila taasisi haina budi
kuvizingatia katika usafirishaji, huduma na urejeshaji nyumbani wa
mahujaji? Pia ingekuwa bora mkatengeneza utaratibu wa ushirikiano baina
ya taasisi zote. Kufanya hivyo kunaweza kusaidia kunyoosha mambo pale
yanapokuwa hayaendi vizuri. Inawezekana pia kwamba kupitia ushirikiano
huo mnaweza kuandaa usafiri wa pamoja na huduma za pamoja kwa mahujaji
wenu wawapo Makka na Madina na hivyo kupunguza gharama.
Ushirikishwaji Masuala ya Kitaifa
Mheshimiwa Mufti;
Tumeipokea
rai yenu ya kutaka Serikali iyatambue na kuyashirikisha mashirika ya
dini kwenye mambo muhimu yahusuyo maslahi ya taifa kabla ya kutekelezwa.
Rai hiyo ni njema na tutaizingatia. Hata hivyo, napenda kuwahakikishia
viongozi wa dini zote na waumini wao kuwa hiyo ndiyo sera na utaratibu
wa Serikali kwa miaka mingi na haujabadilika. Kama itatokea kutofanyika
ni upungufu wa bahati mbaya au wahusika Serikalini ni wageni au
wazembe.
Kwa suala hili la mchakato wa Katiba mpya
nilikwishaeleza kuwa viongozi wa dini watashirikishwa katika hatua zote
muhimu tangu kutoa maoni kuhusu masuala ya kuunda Tume, kwenye Tume
yenyewe, mjadala, Bunge la Katiba na katika kura ya maoni.
Mheshimiwa Mufti;
Pamoja
na ushirikishwaji huo napenda kurudia rai au tahadhari niliyoitoa
wakati wa mkutano wangu na Maaskofu walio Wajumbe wa Jukwaa la Wakristo
Tanzania tarehe 22 Julai, 2011 jijini Dar es Salaam. Niliomba tujitahidi
kuhakikisha kuwa mjadala wa Katiba haugeuki kuwa mdahalo au malumbano
kati ya Wakristo na Waislamu kuingiza maslahi ya dini zao katika Katiba.
Tukiufikisha hapo, kutatokea mivutano ambayo ni migumu kuipatia majibu
na kuna hatari ya Katiba mpya kushindikana kupatikana au kuchelewa sana
na hata amani kuvunjika. Inaweza kuwa ndiyo mwanzo wa umoja wa taifa
letu tulioujenga kwa takriban nusu karne kuvurugika kwa namna ambayo
itakuwa vigumu kuujenga tena. Napenda kuona wote wanapata fursa ya
kushiriki kwa lengo la kuhakikisha kuwa Tanzania inabaki kuwa nchi ya
watu wa dini zote, wenye umoja miongoni mwao. Tanzania inaendelea kuwa
haina dini ingawaje raia wana dini na uhuru wa kuabudu umehakikishwa na
kulindwa ndani ya Katiba kwa mujibu wa na Sheria za nchi. Hali
linawezekana kama viongozi wa dini tutataka kwa dhati iwe hivyo.
Shule za Taasisi za Kiislamu
Mheshimiwa Mufti; Ndugu Zangu Waislamu na Watanzania Wenzangu;
Nimesikia
maelezo na maombi yenu kuhusu shule zilizokuwa zinamilikiwa na taasisi
za Kiislamu zilizotaifishwa na Serikali baada ya Uhuru. Ni kweli kwamba
mara baada ya Uhuru shule zote za msingi, sekondari na vyuo vilivyokuwa
vinamilikiwa na mashirika ya dini na jumuiya za kijamii zilitaifishwa.
Ni kweli pia chache kati ya hizo zilirejeshwa kwa wamiliki wa awali
katika miaka ya 1990. Ni kweli vile vile, kwamba mashirika ya dini
ikiwemo BAKWATA na jumuiya za kijamii zimekuwa zikiomba kurudishiwa
shule hizo lakini Serikali haijayakubali maombi hayo.
Mheshimiwa Mufti; Waheshimiwa Masheikh;
Katika
mkutano wangu wa tarehe 22 Julai, 2011 na Jukwaa la Wakristo suala hili
lilijitokeza na nililitolea ufafanuzi ambao napenda nirudie kuueleza
hapa leo. Baba wa Taifa na Rais wa Kwanza wa nchi yetu, Mwalimu Julius
Nyerere aliamua kutaifisha shule zote za mashirika ya dini na jumuiya za
kijamii hasa za Wahindi na Wazungu kwa lengo la kutoa fursa sawa ya
kupata elimu kwa watoto wa dini zote, wasiokuwa na dini na wa rangi zote
bila kubaguliwa.
Kutokana na uamuzi ule hakuna mtoto
aliyebaguliwa kupata elimu kwa sababu ya rangi yake au dini yake. Hata
wale waliotoka kwenye jamii ambazo kwa dini zao au rangi zao hawakuwa na
shule kabisa au walikuwa nazo kidogo waliweza kupata nafasi, bora tu
wawe na sifa stahiki hasa za kufaulu mitihani na nyinginezo. Lakini si
hivyo tu, ili kujenga usawa kwa upande wa sekondari Mwalimu alikwenda
mbali zaidi. Serikali iligawa sawia nafasi za kwenda sekondari kwa mikoa
na wilaya nchini na siyo tu kufuata kigezo cha mtu kufaulu mitihani.
Mheshimiwa Mufti;
Baada
ya kutaifisha shule hizo, ukiacha shule za msingi zilizojengwa karibu
kila kijiji, Serikali haikuwekeza sana katika ujenzi wa shule mpya za
sekondari. Matokeo yake wakati ule katika mikoa yetu, ukizungumzia shule
za sekondari za Serikali, kwa kweli nyingi, kama siyo zote, ni hizi
zilizotaifishwa kwani Wakoloni hawakuacha shule nyingi na Serikali
haikujenga nyingi mpya. Kwa kweli uwekezaji uliongezeka kwa wingi sana
kwa shule za sekondari za Serikali katika Awamu ya Nne kwa ujenzi wa
Sekondari za Kata.
Kwa kutambua ukweli kwamba shule za Serikali
ni kidogo hata baada ya Serikali kutiliana saini Itifaki ya Makubaliano
(MoU) na TEC na CCT mwaka 1992, kasi ya kurejesha shule ilikuwa ndogo
sana na baadae ikasimama kabisa. Kilichosimamisha ni ule ukweli kwamba
zingerudishwa zote Serikali ingejikuta kama vile haina shule za
sekondari na badala yake shule zingekuwa mikononi mwa makanisa. Kitendo
hicho kingezua manung’uniko na mgogoro katika jamii hasa baada ya zaidi
ya miaka mingi shule hizo kuwa mali ya Serikali. Kwa ajili hiyo, pamoja
na nia njema iliyokuwepo ya kuziboresha na kuziendeleza uamuzi huo
ulikuwa mgumu kutekelezeka. Serikali ikajipa dhima ya kuziboresha na
kuziendeleza.
Mheshimiwa Mufti; Viongozi wa Dini Zote;
Ushauri
na maombi yetu kwa BAKWATA na mashirika mengine ya dini na jumuia
zilizokuwa na shule wafikirie kuwekeza katika ujenzi wa shule na vyuo
vipya badala ya kuendelea kudai shule zao za zamani. Ahadi kubwa ya
Serikali inayotoa kwenu ni kuwa hazitataifishwa tena.
Dawa za Kulevya
Mheshimiwa Mufti;
Kuhusu
dawa za kulevya, sina budi kuwashukuru kwa msimamo wenu wa kutambua
kuwepo tatizo na utayari wenu wa kushirikiana na Serikali katika
mapambano haya. Msimamo huo unanipa faraja kwani kwa kweli tatizo ni
kubwa sana. Sisi katika Serikali tumejipanga vizuri na tumeongeza sana
nguvu ya kupambana na uovu huu. Tunapata mafanikio lakini kazi iliyo
mbele yetu ni kubwa sana inayohitaji ushirikiano wa jamii nzima wakiwemo
viongozi wa dini na waumini wao. Na huo ndiyo ujumbe wangu wa msingi
nilioutoa Mwanza tarehe 29 Mei, 2011 wakati wa kuwekwa Wakfu Askofu
Albert Jella Randa wa Kanisa la Mennonite na Mbinga tarehe 5 Juni, 2011
wakati wa kuwekwa Wakfu Askofu John C. Ndimbo wa Kanisa Katoliki Jimbo
la Mbinga.
Bahati mbaya sana nilipoelezea masikitiko yangu kwamba
hata baadhi ya watumishi wa Mungu wanajihusisha na biashara hiyo,
imeeleweka ndiyo sivyo na kutafsiriwa isivyo. Ni kweli kama walivyoeleza
vyema watu wanaoshughulikia tatizo hili, kwamba miongoni mwa
waliokamatwa na kufikishwa Mahakamani wamo watumishi wa Mungu wa wa
ngazi mbalimbali wa dini zetu zote. Hakuna Askofu wala Sheikh mzito.
Napenda
kuwahakikishia kuwa mimi nitakuwa mtu wa mwisho au kutoa maneno ya
kejeli kwa kuwashutumu watumishi wa Mungu. Kwanza sina sababu ya kufanya
hivyo, lakini pia ninawaheshimu sana. Hata hivyo, nawiwa na wajibu
kupeana taarifa na kutahadharishana na kuomba tushirikiane pale ukweli
unapoonekana.
Nirudie kuwaomba viongozi wa dini zote tushirikiane na
tusaidiane katika mapambano haya ambayo ni yetu sote. Ni jambo lenye
maslahi mapana kwa taifa letu, leo na hasa kesho na kesho kutwa kwani
walengwa na waathirika wakubwa wa dawa za kulevya ni watoto na vijana
wetu ambao ndiyo warithi wetu na taifa la kesho.
Mahakama ya Kadhi
Mheshimiwa Mufti;
Kuhusu
mchakato wa kuanzisha Mahakama ya Kadhi, nimeyasikia maoni yenu kwamba
kumekuwa na kulegalega kwa upande wa Serikali jambo linalowafanya
muingiwe na wasiwasi kuhusu nia njema ya Serikali katika mchakato huu.
Napenda kuwatoa hofu kuwa hakuna kulegalega wala kubadilika kwa dhamira
ya Serikali. Msimamo wa Serikali upo pale pale. Huu ni uamuzi uliofanywa
na Chama chetu na Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya uongozi wa Rais
Benjamin Mkapa wa kutaka kulitafutia ufumbuzi suala la Mahakama ya Kadhi
na kuachiwa Serikali ya Awamu ya Nne kutekeleza.
Na sisi katika
kufuatilia utekelezaji wa jambo hili tulikabidhi Tume ya Kurekebisha
Sheria kuishauri Serikali. Ushauri wa Tume hiyo ulikuwa kwamba Serikali
haiwezi kuunda Mahakama ya kushughulikia masuala ya kidini ya dini
fulani. Jambo hilo liachiwe Waislamu wenyewe kufanya.
Serikali
imekubali ushauri huo na ndipo mchakato ukaanza na tukaunda Kamati ya
pamoja iliyojumuisha Serikali na BAKWATA. Nia ya Serikali ni
kujihakikishia kuwa hicho kitakachoundwa hakiendi nje ya masuala ya
kidini yaani ndoa, takala, mirathi na wakfu kwa mujibu wa dini ya
Kiislamu. Katu si Mahakama ya kushughulikia masuala ya jinai au madai.
Haitajihusisha na masuala ya wizi na kutoa adhabu kama vile za kukatwa
mikono. Haitahusika na kesi za fumanizi na hivyo kutoa hukumu ya kuuawa
mkosaji kwa kupigwa mawe. La hasha !! Narudia kuwa mamlaka yake yatahusu
ndoa, takala, mirathi na wakfu. Isitoshe Muislamu hatazuiliwa kuamua
kutumia sheria za nchi kwa masuala hayo akipenda kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mufti, Waheshimiwa Masheikh, Ndugu Zangu Waislamu;
Napenda
kuwatoa hofu pia kwamba hakuna mkono wa mtu wapo mnadhania hivyo.
Maana, tunajuana. Si ajabu kuna hisia kuwa huenda Kanisa limeingilia
kati kuzuia au kuchelewesha. Siyo hivyo hata kidogo. Tarehe 22 Julai,
2011 nilipoalikwa kuzungumza na Maaskofu katika kikao chao cha Jukwaa la
Wakristo katika risala yao kwangu kuhusu suala la Mahakama ya Kadhi
walitoa ushauri ufuatao kuwa:
“Kuanzisha Mahakama ya Kadhi nchini na
jambo zuri linalowahusu Waislamu. Kwa kuwa ni jambo la kidini waachiwe
Waislamu wenyewe walifanye ndani ya Uislamu, pasipo kutumia hazina ya
Serikali ambayo ni fedha ya walipa kodi wote nchini”
Hiyo ni nukuu kutoka ibara ya 6 ya Risala yao kuhusu Uhuru wa Kuabudu na dhana ya Udini.
Katika
maelezo yangu kwao, niliwahakikishia kuwa mawazo yao yanawiana na yale
ya Serikali kama ilivyoshauriwa na Tume ya Kurekebisha Sheria ambayo
Mwenyekiti wake ni Profesa Ibrahim Juma. Mahakama hii itaundwa na
Waislamu wenyewe ndani ya Uislamu wao na wataiendesha wenyewe na
haitagharamiwa na Serikali.
Sheria ya Ndoa
Mheshimiwa Mufti;
Ni
kweli kwamba Serikali inao mpango wa kupeleka Bungeni Muswada wa Sheria
wa kurekebisha Sheria ya Ndoa ya sasa. Napenda kuwahakikishia kwamba
Serikali inatambua nafasi ya dini katika masuala ya ndoa na mirathi. Si
nia ya Serikali kuanzisha ugomvi na madhehebu ya dini kuhusu suala hili
na lingine lolote. Bahati nzuri taratibu za kutunga sheria ni taratibu
zilizo wazi. Hazina usiri kwa upande wa maandishi na nyaraka wala hauna
kificho katika kuzizungumzia. Miswada huchapishwa katika Gazeti la
Serikali kwa kila mtu kusoma. Pia kuna utaratibu wa kushirikisha wadau
kutoa maoni yao kabla ya muswada kuwasilishwa na kujadiliwa Bungeni.
Naomba
nishauri kuwa Muswada utakapochapishwa katika Gazeti la Serikali
muusome na mhakikishe kuwa mnaandaa vyema maoni yenu kuhusu vipengele
mbalimbali vya Muswada. Kisha hakikisheni mnashiriki katika mikutano ya
wadau kuwasilisha maoni yenu hasa katika maeneo mnayoona yana migongano
na vitabu vitakatifu. Serikali yenu ni sikivu, naamini maoni yenu ya
kujenga yatasikilizwa na hata kuzingatiwa.
Hitimisho
Mheshimiwa Mufti, Waheshimiwa Masheikh, Waislamu Wenzangu na Wageni Waalikwa;
Nimesema
sana na leo ni sikukuu sipendi kuwapunguzia muda wenu wa kwenda
kusherehekea. Napenda kuwahakikishia kuwa Kiserikali tumejiandaa
ipasavyo kulinda usalama wa mali na maisha ya wananchi katika kipindi
chote cha sikukuu.
Mwisho kabisa nakushukuru tena, Mheshimiwa
Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania kwa kunipa heshima hii kubwa. Nawatakia
Waislam na Watanzania wote kwa jumla sikukuu ya Idd-El-Fitr yenye
furaha na faraja tele. Nawaomba tuisherehekee kwa amani na salama. Eid
Mubarak!!
Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania
Assalam Aleykum Warahmatullahi Taala, Wabarakatuh.
Asanteni Sana kwa kunisikiliza
HOTUBA YA MH. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE BARAZA LA EID-EL-FITR, DODOMA,
Written By Admin on Thursday, September 1, 2011 | 12:56 PM
Labels:
NEWS,
TOP STORIES
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment