CCM wajipanga kumwokoa JK

Written By Admin on Monday, August 30, 2010 | 10:21 AM


SIKU moja baada ya Chadema kutangaza nia ya kumwekea pingamizi mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete, chama hicho tawala kimesema kuwa kinajipanga kumwokoa mgombea wake dhidi ya hoja za kutaka mgombea huyo aondolewe mapema.
Juzi, Chadema ilitangaza nia ya kuwasilisha pingamizi kwa Msajili wa Vyama vya Siasa na kwamba ilitaka jana kumwekea pingamizi Kikwete kwa kuwa amekiuka sheria ya gharama za uchaguzi kwa kutangaza nyongeza ya mishahara ya wafanyakazi wa sekta ya umma kwenye mikutano ya kampeni.

                 Kikwete alishaeleza mapema kuwa serikali haiwezi kutekeleza mapendekezo ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) la kutaka kima cha chini cha wafanyakazi wa sekta ya umma kuwa Sh315,000 na hata shirikisho hilo liliposhusha madaio yake hadi Sh260,000, serikali ilisema haina uwezo huo.
Lakini katika siku za karibuni ilibainika kuwa mishahara ya wafanyakazi wa serikali imepanda kwa asilimia kubwa kiasi cha kima cha chini kufikia karibu "pendekezo la pili la Tucta", na Kikwete amekuwa akieleza hayo kwenye kampeni zake kama moja ya hatua zinazoonyesha serikali inawajali wafanyakazi.
Jana, Chadema haikuwasilisha pingamizi hiyo kama katibu wake mkuu, Dk Willibrod Slaa alivyoagiza na msemaji wa chama hicho alieleza baadaye kuwa wanaendelea kupokea malalamiko kutoka maeneo ambayo Kikwete anapita kwenye kampeni zake na hivyo watayajumuisha kwenye pingamizi hilo.
"Tumepokea maoni kutoka kwa watu wa kada mbalimbali waliokerwa na matukio mengine ya Dar es salaam, Mwanza na Kagera ambayo pamoja na ahadi na maelekezo aliyotoa (Kikwete), ametoa pia fedha taslimu au kutumia mali za serikali wakati wa kampeni kinyume cha taratibu," alisema kaimu katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika.
          Aliendelea kusema: "Tumeielekeza kurugenzi yetu ya sheria iandae malalamiko na pingamizi lenye kugusa masuala yote zaidi ya suala la wafanyakazi."
Mnyika alisema jana hawakupeleka pingamizi hilo kwa msajili kwa kuwa wanapata wapate fursa ya kuunganisha suala walilolilalamikia awali la wafanyakazi na masuala mengine ya ukiukwaji wa sheria, kanuni na maadili
Wakati Chadema ikijipanga kuongeza uzito kwenye pingamizi lao, mratibu wa kampeni za CCM, Abdulrahaman Kinana akihojiwa na kipindi cha Nyota ya Asubuhi kilichorushwa hewani jana asubuhi na Televisheni ya Mlimani, alisema CCM haitishwi na pingamizi hilo kwa kuwa "ina ushahidi wa kutosha wa kujibu hoja za Chadema".
Alisema wana ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa hakukuwa na ukiukwaji wowote wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi, ambayo Rais Kikwete aliipitisha kwa mbwembwe mapema mwaka huu akitaka itumike kwenye uchaguzi huu.
"Ingekuwa ni kitu ambacho si halali kama mgombea angesema kuwa akishachaguliwa ndiyo ataongeza mshahara," alisema Kinana na kuongeza kuwa ni muhimu Chadema wakaacha kuhangaika bali waanze kunadi sera zao kwa wananchi.
"Chadema wanadi sera na si kuhangaika," alisema Kinana.
Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa aliliambia gazeti hili jana kuwa anasubiri pingamizi hilo la Chadema na akilipata atakaa na wanasheria wake, kulijadili na kulitolea ufumbuzi.
           Juzi katibu mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa aliwaambia waandishi wa habari kuwa Kikwete amekiuka sheria hiyo kwa kutangaza ongezeko la mishahara ya wafanyakazi wa sekta ya umma akiwa kwenye mikutano ya kampeni.
"Wanasheria wetu wanashughulikia suala hilo kwa kusaidiana na naibu katibu mkuu, John Mnyika kukamilisha pingamizi hilo kwa msajili wa vyama vya siasa," alisema Dk Slaa. 

Dk Slaa alidai kuwa Kikwete alikiuka kipengele cha 6, sehemu ya 21 (1) cha sheria hiyo inayotoa tafsiri ya mambo yanayokatazwa wakati wa mchakato wa uteuzi wa wagombea na kampeni za uchaguzi.
Alisema Kikwete amekiuka kifungu hicho kwa kutangaza ongezeko la mishahara ya wafanyakazi akiwa katika majukwaa ya kampeni, jambo ambalo linaweza kutafsiriwa na sheria hiyo kuwa ni rushwa ya uchaguzi.
Alieleza kuwa Kikwete amekiuka sheria hiyo kwa kuwa yeye kama mgombea, hana mamlaka ya kuongeza mshahara wa wafanyakazi katika kipindi hiki cha kampeni.
"Kwa kutungwa kwa Sheria ya Gharama za Uchaguzi na kusainiwa  Julai 17 mwaka huu pamoja na marekebisho yake, tulitegemea kungesaidia kuleta mabadiliko," alisema Dk Slaa ambaye kitaaluma amebobea kwenye sheria.
"Kitendo cha Kikwete kukiuka sheria hiyo kimenishtua sana.  Watanzania tungependa kupewa ufafanuzi; fedha hizo za (mishahara) zimetoka wapi na kwa mamlaka ya nani kwa kuwa wenye mamlaka ya kuidhinisha matumzi ya fedha za umma ni Bunge," alisema Dk Slaa.

   Alifafanua kuwa kwa mujibu wa katiba, Bunge ndilo lenye mamlaka ya kuidhinisha matumizi ya fedha ikiwa ni pamoja na ongezeko la mishara kwa wafanyakazi wa umma.
"Kitendo cha serikali kuamuru ongezeko hilo nje ya vikao vya bunge, ni ukiukwaji wa sheria za nchi na ndio mwanya uliosababisha kutoweka kwa fedha za Akaunti ya Madeni ya nje(EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT)," alisema Dk Slaa.

"Sehemu ya tano ya sheria hiyo sura ya 21.-(1) inaweka bayana vitendo vinavyokatazwa wakati wa uteuzi wakati wa kampeni za uchaguzi na inasomeka:
"(a)Kila mtu ambaye kabla au wakati wa kipindi cha kampeni, moja kwa moja au kwa namna nyingine yoyote, kupitia kwa mtu mwingine yeyote au kwa niaba yake, anatoa, anakopesha au anakubali kutoa au kukopesha, au anatoa, anaahidi au kumpatia au anajaribu kumpatia fedha yoyote au kitu chochote chenye thamani, mpiga kura au kwa ajili ya mtu yeyote kwa niaba ya mpiga kura yeyote au kwa ajili ya mtu mwingine yeyote kwa nia ya kumshawishi kupiga kura, au kuacha kupiga kura au kumrubuni mtu yeyote kutendo hicho kwa niaba ya mpiga kura huyo kupiga kura au kuacha kupiga kura katika kura za maoni au uchaguzi wowote;
"Kikwete alisema yeye mwenyewe hahitaji kura za wafanyakazi, na akasisitiza katika hotuba yake iliyoitoa kwa wazee wa Dar es Salaam kuwa serikali haina uwezo wa kulipa mishahara hiyo na kama wanafanya hivyo kwa kushinikiza kigezo cha kura, yeye hazitaki; leo mishahara imeongezeka, fedha hizo zimetoka wapi?Tunataka utueleze matumizi hayo ya fedha za umma kinyume na utaratibu."
Kwa mujibu wa Dk Slaa mgombea urais anapaswa kulinda katiba na sheria zilizopo, ili kulifanya taifa liendelee kuwa katika hali ya amani na utulivu katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu.

             Dk Slaa alisema kuwa kitendo cha rais kutumia nafasi hiyo kutangaza mishahara kwenye kampeni ni kujipa upendeleo kwa kushawishi watu kumpigia kura kwa kutumia nafasi aliyonayo.
             Dk Slaa pia alitumia fursa hiyo kukemea kitendo cha kufanya maamuzi kwa kukiuka sheria zilizopo akieleza kuwa kufanya hivyo kunaweza kuhatarisha usalama wa nchi.
Wakati huohuo, Mahakama Kuu Dar es Salaam imekataa kile kilichoonekana kuwa ni tabia ya upande wa Jamhuri katika kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na mwalimu mstaafu, John Paul Mhozya dhidi ya Rais Jakaya Kikwete.
Katika kesi hiyo Mhozya, 59, ambaye alikuwa mkufunzi  wa Chuo cha Ualimu cha Dar es Salaam, amefungua kesi Mahakama Kuu akitaka Kikwete ambaye pia ni mgombea urais wa CCM, aondolewe kwenye kinyang’anyiro hicho kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
                 Jana, Jaji Agustine Shangwa aliionya serikali dhidi ya ucheleweshaji unaosababisha suala hilo lisishughulikiwe mapema. Jaji Shangwa alisema hayo wakati kutaka kusikiliza pingamizi la awali la kesi hiyo lililowekwa na CCM pamoja na serikali ambazo zinataka shauri hilo litupiliwe mbali.
Kabla ya kuzungumzia ucheleweshaji huo, Jaji Shangwa alizishauri pande zote katika kesi hiyo ziwasilishe hoja zake kwa njia ya maandishi ili kumpa nafasi mlalamikaji kuziandaa kujibu hoja hizo, ushauri ambao ulikubaliwa na pande zote.
Baada ya pande hizo kukubaliana na ushauri huo, Jaji Shangwa aliutaka upande wa Jamhuri ueleze siku ya kuwasilisha hoja zake za na wakili wa serikali, Sylvester Mwakitalu alipendekeza iwe Septemba 27, lakini Jaji Shangwa alikataa tarehe hiyo akisema kuwa ni mbali sana na kuutaka upande wa Jamhuri kufanya kazi ya ziada, ikilazimu kukesha ili kuhakikisha kuwa inawasilisha mapema hoja zake hizo.
“Wakati mwingine hata sisi huwa tunakesha tunafanya kazi ingawa hakuna mtu anayejua kuwa tunakesha," alisema.
Jaji Shangwa alisema kuipeleka kesi hiyo hadi Septemba ni kama kutoutendea haki upande mmoja  na kuitaka Jamhuri iwasilishe hoja zake ndani ya juma moja ili iweze kuisha haraka.

             Kutokana na ushauri huo ilikubaliwa kuwa Jamhuri iwasilishe hoja zake Septemba 6 na Mhozya azijibu Septemba 13. Serikali imetakiwa iwasilishe hoja zake za ufafanuzi Septemba 20 na kesi hiyo itatajwa tena Septemba 21.
Katika kesi hiyo Mhozya anataka Kikwete aondolewe katika kinyang’anyiro hicho akidai kuwa alikiuka haki za kikatiba za Watanzania na kutumia vibaya ofisi yake katika kipindi cha kwanza cha miaka mitano ya utawala wake.
“Amekuwa akiwatumia kuonyesha mamlaka yake; kuonyesha utajiri, kwa safari zake binafsi zisizoisha na starehe zake binafsi,” anaeleza Mhozya katika hati yake aliyoiwasilisha mahakamani hapo wiki mbili zilizopita.
Pia anatuhumu Rais Kikwete kwamba ameonyesha ubaguzi dhidi yake na kukataa kusikiliza ombi lake la kumtaka angalie masuala muhimu yanayohitaji kusimamiwa na rais".
Mwaka 1993 Mhozya aliwahi kufungua kesi akiitaka mahakama kumbana aliyekuwa rais wakati huo, Ali Hassan Mwinyi.
Katika kesi hiyo, ambayo Jaji Barnabas Samatta aliitupilia mbali, Mhozya aliiomba mahakama ikubali kwamba Mwinyi alikuwa na makosa ya kuruhusu kukiukwa kwa katiba na alikuwa na kosa la kujibu kwa kuiruhusu Zanzibar ijiunge na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC).


SOURCE: MWANANCHI

0 comments:

Post a Comment