Mgombea urais kupitia Chama Cha Demokrasia na maendeleo (Chadema), DK. Wilbroad Slaa, amekana kuwa na mahusiano ya kingono na kwamba hajawahi kumtambulisha kwenye halaiki Josephine Mushumbusi, anayedaiwa kuwa mke wa ndoa wa Aminiel Mahimbo, kwamba ni mke wake.
Dk. Slaa, kupitia wakili wake Mabere Marando, amekanusha madai hayo ya fidia ya Sh. bilioni moja, anazodaiwa na Mahimbo kwa tuhuma za kuzini na mke wake.
Akijibu hoja za mlalamikaji dhidi ya kesi ya madai namba 122 ya mwaka huu iliyofunguliwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, kupitia hati iliyowasilishwa mahakamani hapo Septemba 28, mwaka huu, Dk. Slaa amemtaka mlalamikaji kuwasilisha ushahidi utakaothibitisha tuhuma hizo.
Pia, mdaiwa huyo kupitia hati hiyo, amekanusha kuwa pamoja na mke huyo aliyetajwa katika hati ya madai ya tuhuma dhidi yake.
Dk. Slaa amedai kuwa asingeweza kujua kwa hali ya kawaida kwamba mwanamke huyo (Mushumbusi) alikuwa ameolewa na kwamba hakuwahi kumwambia kuwa aliwahi kuolewa.
Hati hiyo, inaeleza kuwa Dk. Slaa alisikia kwa mara ya kwanza kuhusu ndoa ya mdai baada ya kusoma nakala ya kumbukumbu mbalimbali za ndoa hiyo zilizokuwa zimeambatanishwa na hati ya madai ya msingi (ambayo nakala yake alipatiwa) zikieleza kwamba Mushumbusi aliolewa na mdai.
Kutokana na hilo, alidai kuwa mdai amejidhalilisha mwenyewe, kujishusha kwa kutangaza hadithi ya kuhusu ndoa yake kwenye vyombo vya habari nchini.
Dk. Slaa aliendelea kujibu kupitia hati hiyo, kwamba mlalamikaji amejidhalilisha alipokubali kulipwa na chama cha siasa ili achapishe hadithi hiyo ikiwa ni pamoja na kukubali kwenda kuishi na kiongozi mwanamke mwenye wadhifa katika chama hicho cha siasa (chama hicho hakikutajwa kwenye hati hiyo).
Katika madai ya msingi, Mahimbo anadai kunyang’anywa mkewe wa ndoa Mushumbusi na Dk. Slaa na kutokana na hilo, anadai fidia ya Sh. milioni 200 kutokana na hasara alizopata baada ya mdaiwa huyo kumtangaza mkewe wa Ndoa Josephine kuwa mchumba wake ambapo pia anadai Sh. milioni 800 ikiwa ni hasara ya jumla aliyopata.
Mdai huyo anadai kuwa, Septemba 7, 2002 alifunga ndoa na mwanamke huyo katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Ushirika wa Kijitonyama, Dar es Salaam na kuishi naye maeneo mbalimbali likiwemo Kimara, Baruti, Dar es Salaam.
SOURCE: NIPASHE
Dk. Slaa amjibu anayedai amempora mke
Written By Admin on Saturday, October 2, 2010 | 9:05 PM
Labels:
POLITICS,
UCHAGUZI 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
.jpg)
0 comments:
Post a Comment