- Wasema wamejiandaa kukabili vurugu
- Waonya vyama vya siasa, taasisi binafsi
Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo, akitoa tamko la ulinzi na usalama mbele ya waandishi wa habari Makao Makuu ya jeshi hilo jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Naibu Kamishna wa Polisi, Peter Kivuyo, na kulia ni Mkuu wa Operesheni Maalum za Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna, Venance Tossi.
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) likishirikiana na Jeshi la Polisi nchini wamevitaka vyama vya siasa kukubali matokeo baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba na kuonya kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vimejiandaa kikamilifu kupambana na yeyote atakayejaribu kuyakataa matokeo.
Tamko la vyombo hivyo vya usalama lilisomwa mbele ya waandishi wa habari jana na Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo, Makao Makuu ya JWTZ, Upanga, jijini Dar es Salaam.
Katika mkutano huo, Luteni Jenerali Shimbo aliambatana na maofisa kadhaa wa JWTZ, Kamanda wa Kikosi cha Operesheni Maalumu cha Jeshi la Polisi nchini, Venance Tossi, na Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya jinai, Peter Kivuyo.
Alisema wamelazimika kuweka msimamo huo bayana baada ya kuona dalili za baadhi ya taasisi na vyama vya siasa kutaka kuvunja sheria wakati huu wa kampeni.
“Vyombo vya ulinzi na usalama vimejiandaa kikamilifu kupambana na mtu, watu, kikundi, chama au taasisi yoyote itakayokwenda kinyume na (cha) sheria, kuchochea au kufanya fujo, kuvunja amani kwa mujibu wa sheria. Aidha, kuchochea kuyakataa matokeo,” alisema Luteni Jenerali Shimbo.
Aliongeza kuwa: “Vyama vya siasa vifanye kampeni kwa ustaarabu na kufuata sheria na kanuni za uchaguzi, visitukane vyombo vya dola wala kuvichokoza kwa vile havihusiki na siasa zaidi ya kulinda amani na utulivu.”
Alisema vyombo vya ulinzi vimejipanga kuhakikisha kwamba damu haimwagiki wakati wa kampeni na baada ya uchaguzi na kuwaomba wananchi kushirikiana navyo katika kutunza amani na usalama wa nchi.
“Dalili zimeanza kuonekana za kutaka kuvunja sheria katika kampeni, kuchochea fujo na uvunjifu wa amani ... dalili hizi sio nzuri na zinaweza kuharibu utulivu na amani iliyopo kwa miaka mingi. Aidha, baadhi ya mashirika yameanza kutoa matamko yanayolenga kushabikia vyama vya siasa na wagombea,” alisema.
Luteni Jenerali Shimbo alisema vyombo vya ulinzi na usalama vimebaini pia kwamba baadhi ya taarifa zinazotolewa kwenye vyombo vya habari hazichujwi ipasavyo.
Aliwataka waandishi wa habari kuchuja taarifa zao. “Ninyi pia mnayo dhamana kubwa ya kulinda amani na utulivu, wananchi wanafuatilia sana vyombo vya habari mkiruhusu haya mtatupa kazi kubwa sana, hamtakuwa mmelitendea haki taifa hili,” alisema Shimbo.
Bila kutaja chama chochote, alisema baadhi ya vyama vya siasa vimekuwa vikivihusisha vyombo vya ulinzi kwa kuvihusisha na vyama vingine vya siasa.
Alisisitiza kuwa maofisa wa vyombo hivyo hawafungamani na chama chochote na kwamba hawaruhusiwi kushabikia upande wowote zaidi ya kuhakikisha taifa lipo salama.
“Vyombo vya ulinzi na usalama vinapenda kueleza kuwa wajibu wake ni kuhakikisha amani, usalama na utulivu wa nchi yetu wakati wowote usiku na mchana, havifungamani na chama chochote cha siasa bali vinatii viongozi na serikali iliyoko madarakani,” alisema.
Alisema vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kulinda amani wakati huu wa kampeni, siku ya kupiga kura na wakati wa kuapishwa.
Tamko hili la vyombo vya ulinzi na usalama limekuja zikiwa zimesalia siku 29 tu kabla ya siku ya kupiga kura, Oktoba 31, mwaka huu.
Mnyika: Uchaguzi ni kazi ya Polisi
Akizungumzia tamko hilo, Kaimu Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, alisema chama hicho kinaamini kwamba JWTZ ni jeshi la wananchi ambalo lina jukumu kubwa la kulinda mipaka ya nchi ili kuhakikisha ni salama wakati wote.
Alisema jukumu la uchaguzi linalihusu Jeshi la Polisi ambalo linasimamia amani kwenye vituo vya kupigia kura pamoja na NEC ambacho ni chombo cha serikali kinachohusika na uchaguzi.
“Tunajua JWTZ halina chama, lakini maofisa wake wanaweza kushiriki kwenye zoezi la upigaji kura kwa kiongozi wanayemtaka sio vizuri kwa jeshi letu kujiingiza kwenye siasa hasa kipindi hiki, tunadhani JWTZ lingeliachia jeshi la polisi jukumu la kulinda amani wakati wa uchaguzi,” alisema.
Mnyika alifafanua kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kukishauri chama tawala kikubali matokeo kwa kuwa mara nyingi vyama tawala vimekuwa na kasumba ya kutokubali kushindwa.
Alisema amani na utulivu wakati wa uchaguzi unategemea usimamizi mzuri wa NEC kwa kuweka uwanja sawa wa kampeni na upigaji kura.
Makamba: Sijui yanayoendelea Dar
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba, alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa hakuwa amepata taarifa kwa kina.
“Mimi nipo Tunduru sijui mambo yanayoendelea huko...niulize ya Tunduru siwezi kuzungumzia kitu ambacho sijakisikia,” alisema.
Kinana: Tutafuata sheria
Meneja Kampeni wa CCM, Abdulrahman Kinana, alipotakiwa kutoa maoni naye alisema CCM itazingatia sheria, kanuni na taratibu zote zinazotawala uchaguzi na kwamba chama hicho kitaheshimu matokeo ya uchaguzi yatakayotangazwa na NEC.
“Lakini kama kutakuwa na malalamiko yoyote tutafuata taratibu zilizowekwa kuyawasilisha kwa vyombo husika,” alisema.
Alisema chama hicho kinategemea pia kwamba vyama vingine vya siasa vitazingatia sheria na kanuni ili kudumisha amani wakati huu wa kampeni na baada ya uchaguzi mkuu.
CHANZO: NIPASHE
JWTZ na Polisi, watoa tamko Uchaguzi Mkuu
Written By Admin on Saturday, October 2, 2010 | 9:14 PM
Labels:
POLITICS,
UCHAGUZI 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment